2 Chronicles 9

Malkia Wa Sheba Amtembelea Sulemani

(1 Wafalme 10:1-13)

1 aMalkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Sulemani, huyo malkia akaja Yerusalemu kumjaribu kwa maswali magumu. Alifika akiwa na msafara mkubwa sana, pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani, alikuja kwa Sulemani na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake. 2Sulemani akamjibu maswali yake yote, wala hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwake asiweze kumwelezea. 3 bMalkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, 4chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika Hekalu la Bwana alipatwa na mshangao.

5Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli. 6 cLakini sikuamini yaliyosemwa hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana kuliko ile taarifa niliyoisikia. 7Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wasimamao mbele yako daima na kusikia hekima yako! 8 dAhimidiwe Bwana Mwenyezi Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe, na akakuweka juu ya kiti chake cha ufalme utawale kwa niaba ya Bwana Mwenyezi Mungu wako. Kwa sababu ya upendo wa Mungu wako kwa Israeli na shauku yake ya kuwadhibitisha milele, amekufanya wewe mfalme juu yao, ili kudumisha haki na uadilifu.”

9 eNaye akampa mfalme talanta 120
Talanta 120 za dhahabu ni sawa na tani 4.5.
za dhahabu, kiasi kikubwa cha vikolezi na vito vya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa vikolezi vizuri kama vile Malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Sulemani.

10 g(Watumishi wa Hiramu na wa Sulemani wakaleta dhahabu kutoka Ofiri, tena wakaleta shehena kubwa ya miti ya msandali na vito vya thamani. 11Mfalme akatumia hiyo miti ya msandali kuwa ngazi kwa ajili ya Hekalu la Bwana na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha msandali hakijawahi kuingizwa Yuda tangu siku ile.)

12Mfalme Sulemani akampa Malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, zaidi ya vile alivyokuwa amemletea mfalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.

Fahari Ya Sulemani

(1 Wafalme 10:14-25)

13Uzito wa dhahabu ambayo Sulemani alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta 666,
Talanta 666 za dhahabu ni sawa na tani 25.
14 imbali na mapato yaliyoletwa na wafanyabiashara na wachuuzi. Wafalme wote wa Arabuni na watawala wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha.

15Mfalme Sulemani akatengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa. Kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli 600
Shekeli 600 za dhahabu ni sawa na kilo 3.5.
16 kAkatengeneza pia ngao ndogo 300 za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu
Mane tatu za dhahabu ni sawa na kilo 1.7.
za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.

17 mKisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi. 18Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na mahali pa kuwekea miguu vyote vya dhahabu. Pande zote za kiti kulikuwa na mahali pa kuegemeza mikono, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono. 19Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wowote. 20Vikombe vyote vya Mfalme Sulemani vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo wakati wa Sulemani. 21 nMfalme alikuwa na meli nyingi za biashara
Au: za Tarshishi (ona pia 1 Fal 10:22; 22:48; 2 Nya 20:36; Isa 2:16; 60:9).
baharini zilizoendeshwa na watu wa Hiramu. Kwa mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wakubwa na wadogo.

22 pMfalme Sulemani alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia. 23 qWafalme wote wa dunia wakatafuta kukutana na Sulemani ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake. 24 rMwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja, alileta zawadi, vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezi, farasi na nyumbu.

25 sSulemani alikuwa na mabanda 4,000 kwa ajili ya farasi na magari ya vita, farasi 12,000 ambao aliwaweka katika miji ya magari ya vita na katika Yerusalemu pamoja naye. 26 tSulemani akatawala juu ya wafalme wote kuanzia Mto Frati mpaka kwenye nchi ya Wafilisti na kuendelea hadi mpaka wa Misri. 27 uMfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu vilimani. 28 vFarasi wa Sulemani waliletwa kutoka Misri na kutoka nchi nyingine zote.

Kifo Cha Sulemani

(1 Wafalme 11:41-43)

29 wKwa habari za matukio mengine ya utawala wa Sulemani, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Nathani, katika unabii wa Ahiya Mshiloni na katika maono ya Ido mwonaji kuhusu Yeroboamu mwana wa Nebati? 30 xSulemani alitawala Israeli yote miaka arobaini, akiwa Yerusalemu. 31 yKisha Sulemani akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa katika mji wa Daudi baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.
Copyright information for SwhKC